Ee Mungu, uniokoe

Ee Mungu, uniokoe, Maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, Pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, Mkondo wa maji unanigharikisha. Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua. Uniponye kwa kunitoa matopeni, Wala usiniache nikazama. Na niponywe nao wanaonichukia, Na katika vilindi vya maji. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, Nami nitamtukuza kwa shukrani.  Nayo yatampendeza Bwana kuliko ng’ombe, Au ndama mwenye pembe na kwato.  Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake. Mbingu na nchi zimsifu, Bahari na vyote viendavyo ndani yake.

Amina

Advertisements

Mtumaini Bwana

Enyi Israeli, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.  Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.  Enyi mmchao Bwana, mtumainini Bwana; Yeye ni msaada wao na ngao yao.  Bwana ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni,  Atawabariki wamchao Bwana, Wadogo kwa wakubwa.

Zaburi 115: 9-13

Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo.  Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi, mtumwa wala mwungwana, bali Kristo ni yote, na katika yote.

Kol 3:5-11

Hekima ni pato bora

Wanangu, yasikilizeni mausia ya baba yenu, Tegeni masikio mpate kujua ufahamu.
Kwa kuwa nawapa mafundisho mazuri; Msiiache sheria yangu.
Maana nalikuwa mwana kwa baba yangu, Mpole, mpenzi wa pekee wa mama yangu.
Naye akanifundisha, akaniambia, Moyo wako uyahifadhi maneno yangu; Shika amri zangu ukaishi. 
Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.
Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. 
Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu. 
Umtukuze, naye atakukuza; Atakupatia heshima, ukimkumbatia. Atakupa neema kuwa kilemba kichwani; Na kukukirimia taji ya uzuri.

Mithali 4:1-9