Omba kwa jina la Yesu, utapata uombayo

Mpendwa ,

Kitu chochote ulichonacho moyoni , ukiomba kwa jina la Yesu, Mungu atakupa. Yesu anasema “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yohana 14:13-14

Lakini ni vema kuomba kwa imani, bila kuona shaka ndani ya moyo wako, kwani ukiwa na shaka ni vigumu kupata unayotarajia. “Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” Marko 11:23-24

Hata hivyo ni vizuri kuzingatia ya fuatayo ili kupata kile unachoomba:

1. Unapoaswa kukaa ndani ya Mungu , ndani ya neno lake “ Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.” Yohana 15:8

2. unapaswa kuomba kama Mungu anavyopenda, Mwambie Mungu mapenzi yako yatimizwe “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.” 1 Yohana 5:14

3. Omba kwa faida ya roho yako na wenzako acha ubinafsi “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu” Yakobo 4:3

Basi Tumwombe Mungu sana, atupe neema za kutambua kuwa anatupenda na anatujalia kila tuombalo, ilimradi tu tufanye mapenzi yake.

Yesu Anatakasa

Ndugu mpendwa,

Kama vile yule mwenye ukoma alivyomuomba Yesu amtakase, nasi tukienda na kumwomba Yesu atutakase, Yesu ni mwema na mwenye huruma , atatutakasa si dhambi zetu tu bali atayatakasa hata maisha yetu ya kila siku. Mwendee Yesu leo mwambie “…Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Matayo 8:2, Naye anajibu kwa upendo “…akisema Nataka; takasika.” Matayo 8:2 , hivyo ndugu toa maisha yako kwa Yesu na mweleze kila lililo moyoni mwako naye atakutakasa.

Tuombe: Bwana Yesu, ukitaka, waweza kunitakasa. Amina

Heri kila mtu amchaye Bwana – Atabarikiwa

Ni vema kufuata amri za Bwana na kutenda apaendayo, kwani baraka zitakuwa juu yako.

Heri kila mtu amchaye Bwana, Aendaye katika njia yake.Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.

Zaburi 128:1-4

Mungu humpenda atoaye kwa moyo wa ukunjufu

Mpendwa katika Bwana,
“Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.” 2 Wakorinto 9:7. Tunapotoa Mungu anapenda tutoe bila manung’uniko, tutoe kwa upendo na shukrani, ndivyo neno la leo linavyotufundisha. Kila wakati tunapotoa iwe ni kwa kumsaidia ndugu au rafiki, au kuchangia katika shughuli za kanisa, tunahitajika kutoa kadiri tulivyokusudia moyoni mwenu bila kulazimishwa na mtu yeyote. Na tunapotoa, tutoe kilicho bora kwani “Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.” 2 Wakorinto 9:6
Basi tumwombe Mungu atujalie kutoa bila manung’uniko.

Tukiziungama dhambi zetu – Tutasamehewa

Mpendwa,

Kama binadamu tunaweza kuingia dhambini kwa sababu ya udhahifu wetu wa moyo, hakuna asiye na dhambi, lakini Mungu wetu ni mwema sana, anasemhe dhambi kama ukitubu kwa dhati na kuamua kuziacha dhambi zako “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” 1 Yohana1:9, “Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.” Matendo 8 :22

Tuombe:

Mungu mwema, usiangalie udhaifu wangu bali nisameh dhambi zangu na unipe neema ya kushinda vishawishi vya shetani. Amina

repenttubu

Hakuna kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu

Mpendwa,

Mungu ni upendo, na hakuna kinachoweza kututenga na upendo huo, “…katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.  Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,  wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Warumi 8:37-39

Basi kwa kuwa hakuna kinachotutenga na upendo wa Mungu, basi nasi tumpende Mungu.