Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.
Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.
Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.
Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.
Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.
Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.
Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.
Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.
Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.
Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.
Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.
Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.
Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.
Mithali 11:1-13