“Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.”

Matendo ya Mitume 2:36-39

Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?

Mpendwa

Katika wiki Takatifu, leo siku ya Ijumaa kuu, tunakumbuka mateso na kifo cha Bwana Yesu pale Msalabani. Ukisoma injili ya Yohane 18 na 19 sura zote mbili, utaona historia ya jinsi Yesu alivyoteseka kuanzia alipokamatwa, alivyoteswa na kufa pale msalabani. Katika safari hii ya ukombozi kuna mengi ambayo Yesu anatufundisha , kati ya hayo;

La kwanza tunapoamua kumfuata Yesu , tunapaswa kweli kuyatoa maisha yetu kwake, Petro alimua kumfuata Yesu lakini alipoulizwa wewe u mmoja wao, alimkana Yesu na kukataa kabisa, mara tatu anasema hamjui Yesu (Yohana 18:25-27), je wewe mpendwa umeyatoa maisha yako kwa Yesu, na je unapokutana na vikwazo katika kuilinda Imani yako , unamkana Yesu? jitafakali.

Jambo la pili tunalojifunza katika safari ya mateso ya Yesu, ni kuwa na msimamo, unapotaka kufanya maamuzi ya jambo fulani usiangalie macho ya watu, kama wewe hujayatoa maisha yako kwa Yesu na uanataka kufanya hivyo basi usiangalie macho ya watu. Baada ya mahojiano na Yesu, Pilato aliona kabisa kuwa hana kosa, lakini aliyaogopa macho ya watu na akamhukumu afe (Yohana 19:4-19). Je wewe unapotaka kutenda mema unaogopa macho ya watu?

Tumwombe Mungu basi katika siku ya leo atupe ujasiri wa kutenda kadiri ya mapenzi yake.

Video Courtesy: YouTube

Nimewapa kielelezo nanyi mtende vivyo

Leo ni siku ya Alhamis kuu, katika wiki Takatifu. Leo Yesu anaonyesha na anatufundisha upendo mkuu. Katika hali ya kawaida unapokuwa na msaidizi wa kazi katika nyumba yako, ni yeye ndiye ayekusadia kazi ikiwamo pengine hata kukunawisha mikono kabla na baada ya kula, lakini je unaweza wewe ukaamka siku moja na kumwambia msaidizi wako wa kazi za ndani kaa hapo, ukamnawisha mikono na kumwambia kula, na baada ya kula ukamnawisha mikono vile vile?! Ni kitu ambacho kitakuwa cha kipekee sana. Ndivyo Yesu alivyofanya kwa wanafunzi wake, yeye kama mwalimu , wanafunzi wake walipaswa kumtii na kumsadia , lakini Yeye ananinuka na kuwatawadha miguu “Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga.” Yohana 13:3-5.  Ni upendo wa aina ya pekee kwa mtu aliye mkubwa kumtwadha mdogo katika jamii ya Yesu. Nasi twafundiswa kuwa na upendo kwa wengine, haina maana tuwatawadhe miguu watu wengine, ila tutende yale matendo ya upendo, kwani ndivyo Yesu alivyofanya na alivyoagiza “Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” Yohana 13:13-15.

Mpendwa, tumwombe Bwana, nasi tukayatende ule upende aliotuonyesha kam kielelezo, na hasa katika kuwasaidia wasijiweza, kuacha dhuruma, kufanya kazi kwa bidii na kusali daima. Mungu akubariki katika siku hii na uwe na upendo wa juu kama Bwana alivyotufundisha.

courtesy: https://www.lds.org/bible-videos/videos/the-last-supper?lang=eng

Courtesy YouTube

Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?

“Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.” Matayo 26:14-25

Mpendwa, ni wapi utakapomuandalia Yesu Pasaka? andaa Pasaka katika familia yako ambapo hutamhuzunisha Yesu wana kumsaliti kwa matendo maovu.

Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti

Mpendwa,

Tupo katika wiki takatifu, au wiki kuu, au juma kuu ama wiki ya mateso, katika siku ya leo neno linatuongoza kutafakari ni jinsi gani Yesu anavyohuzunika kwa kuona mmoja wa wale wanafunzi anaowapenda anakwenda kumsaliti “Naye alipokwisha kusema hayo, Yesu alifadhaika rohoni, akashuhudia akisema, Amin, amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti … Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote.” Yohana 13:21, 26. Mpendwa Yesu alikubali kuteswa ili kutukomboa sisi, lakini je bado unamsaliti mpaka leo kama alivyofanya Yuda Iskariote? Kumsaliti Yesu ndiko kutenda dhambi au kuenenda kinyume na amri za Mungu; kutoa au kupokea rushwa, matukano, kusengeja, hasira , uzinzi, wizi na kila baya la dunia, kufaya hayo yote ni kumsaliti Yesu. Basi tugeuke, hasa katika wiki hii kuu, tutafakari mateso ya Bwana Yesu na kuacha dhambi, kuanzia sasa na siku zote za maisha yetu.

 Tuombe neema za Roho Mtakatifu ili tuweze kushinda vishawishi na kuishi kwa kutenda matendo mema.

Hosana! Amebarikiwa Yeye ajaye kwa Jina la Bwana!

Kisha wakamleta huyo mwana punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani.

Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,

Hosana! Amebarikiwa Yeye ajaye kwa Jina la Bwana!

Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!

Hosana kwake Yeye Aliye Juu!

Marko 11:7:11

courtesy: http://wordforlifesays.com/2015/03/23/hosanna-to-the-coming-king-sunday-school-lesson-mark-111-11-march-29-2015/

Mkavae utu mpya, msitende dhambi

Mpendwa,

Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani. Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo; ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi. Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

 Waefeso 4: 17,19-32