Sala yangu leo

Bwana, moyo wangu hauna kiburi, Wala macho yangu hayainuki. Wala sijishughulishi na mambo makuu, Wala na mambo yashindayo nguvu zangu. Hakika nimeituliza nafsi yangu, Na kuinyamazisha. Kama mtoto aliyeachishwa Kifuani mwa mama yake; Kama mtoto aliyeachishwa, Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu.Zaburi 131:1-2

Mshirikishe Mungu Kabla hujafanya maamuzi,

Mpendwa,

Yesu kabla ya kuchagua mitume wake, alichofanya ni kukesha akiomba, ili awachague wale wanaofaa kuwa mitume, neno linatuambia “Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume;” Luka 6:12-13. Mpendwa, kama Yesu mwenyewe ambaye ni Mungu Kweli aliomba kabla ya kufanya maamuzi ya kuwachagua mitume, sembuse wewe na mimi? Basi kabla hujafanya maamuzi ya jambo lolote, liwe kubwa sana ama dogo sana, ni vema ukamshirikisha Mungu kwa kumwomba. Na jambo lingine Yesu analotufundisha, unapofanya maombi kama haya ya maamuzi ni lazima uwe mahali patulivu, na ndiyo maana Yeye Yesu alipanda mlimani, pasi nawe mlima wako ni sehemu tulivu, na hasa utulivu wa moyo wako, na utulivu ulio mkuu, ni kutokua na mawaa rohoni mwako, hasa kutokuwa na kinyongo, chuki na dhambi ya aina yeyote, kuwa safi rohoni kunafanya Mungu asikie maombi yako.

Tumwombe Mungu basi atupe nafasi ya kuomba kabla ya kufanya maamuzi katika kila jambo linalotukabili.

jesus
courtesy: bessg.wordpress.com

Maisha ni Kukesha

Mpendwa,

Nakusalimu kwa Upendo mkuu,

Neno la leo linatukumbusha kukesha. Unapokesha kwa maana ya kawaida ni kuwa macho usiku kucha kwa dhumuni Fulani, yaweza ukawa unalinda mji wako ama jambo lolote lingine. Yesu leo anatumbia tukeshe, kwani maisha yetu yanaweza kwisha wakati tusioujua na tukarudi kwa Baba wa Milele, “Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu.”  Luka 12:39-40. Kukesha huku anakosema Yesu ni kutenda mema kila siku na kufanya mambo yale yanayompendeza Mungu. Kumbuka Mungu atakapokuja na kukuta unayatenda mapenzi Yake, anatoa malipo kwa kila jema unalotenda kwa kiwango cha uelewa wako wa kutenda hayo “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi. Luka 12:47-48

Basi mpednwa Tumwombe Mungu sana atupe nguvu ya kukesha bila kuchoka,

Je Mungu , ametenda jipya kwako?

Mpendwa,

Mungu anasema “Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. “ Isaya 43:19, hebu jitafakari leo na uone ni lipi jipya Mungu amelitenda kwako, inaweza ikawa kila siku tunaomba bila kufikiri vema, kumbe kuna mengi ambayo Mungu ameyatenda kwetu, kukaa kimya na kutafakari ni vizuri ili kujua ni mema mangapi Mungu amekutendea. Barikiwa Sana leo

Msiyatafakari mambo ya zamani

Mpendwa,

Siku zote, jambo likishafanyika kama ni zuri shukuru Mungu, kama ni baya shukuru Mungu vile vile, ila unapaswa kujua kuwa hautakiwi kuhuzunika kwa yale magumu yanayotokea katika maisha, kwani Mungu wetu ni mwena na anatufanyia njia  na kututendea mapya na mema zaidi yatakayotufariji “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.  Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. ” Iasya 43:18-19

Mungu akubariki

Usiache Upendo wa Mungu

Mpendwa,

Nakusalimu katika jina la Yesu, Amina.

Mungu anapenda sana kila mmoja tumtolee, lakini kutoa kwetu kutakuwa na faida tu endapo tuaweka upendo kwa wenzetu kwanza, tunapaswa kutosahau kuwapenda na kuwajali wenzetu, kwa namna hiyo ndipo kutakuwa na faida kwa matoleo na zaka zetu. Yesu anaonya wale ambao wanapenda kutoa lakini hawana upendo; “Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.” Luka 11:42. Basi tumwombe Mungu atupe nguvu ya kufanya yote kwa moyo.