Asante Mungu

Ni neno jema kumshukuru Bwana, Na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu.
Kuzitangaza rehema zako asubuhi, Na uaminifu wako wakati wa usiku.
Kwa chombo chenye nyuzi kumi, Na kwa kinanda, Na kwa mlio wa kinubi.
Kwa kuwa umenifurahisha, Bwana, Kwa kazi yako; nitashangilia Kwa ajili ya matendo ya mikono yako.
Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni mafumbo makubwa.
Mtu mjinga hayatambui hayo, Wala mpumbavu hayafahamu.
Wasio haki wakichipuka kama majani Na wote watendao maovu wakistawi. Ni kwa kusudi waangamizwe milele;
Bali Wewe, Bwana, U Mtukufu hata milele.

Zaburi 92:1-9

Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka

Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai.

Yohana 5:22-25