Ichochee karama ya Mungu

Mpendwa

Unapoikea Imani, unatakiwa uichochee ili ikue, unatakiwa kutokuwa mwoga kwa kulitangaza neno la Mungu wakati wote, hasa kwa kutenda yaliyo mema na kukemea mabaya bila kuogopa. Neno linatuambia “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu” 2 Timotheo 1:6-8

 Mungu akubariki

Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?

Mpendwa,

Katika kila tunalofanya na tunalonena ni lazima tuujue ukuu wa Mungu. Mungu yupo nasi na anatenda mambo makuu sana, hivyo ni wajibu kutomdharau kwa lolote na kumwomba na kumshukuru kwa yote, hakuna anayeweza kuushinda ukuu wa Mungu “ Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi? Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe? Cheo chake ni kirefu kuliko dunia, Ni kipana zaidi ya bahari. Yeye akipita, na kufunga watu, Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia? Kwani yeye awajua watu baradhuli; Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.  Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu, Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu.”  Ayubu 11:7-12

Tumwombe  Mungu atupe Nguvu za kuuona na kutii ukuu Wake.

Amina

Toa ujiweke wakfu kwa Bwana

Mpendwa,

Kumtolea Mungu kunahitaji uhiari na utayari bila kulazimishwa, na unapotoa kwa hiari unajiweka wakfu kwa Bwana, kwamba unayatenga maisha yako na dunia hii na kujitoa kwa Mungu zaidi. Mfalme Daudi aliwaulizwa watu “…Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa Bwana?… Ndipo wakuu wa mbari za mababa, na wakuu wa kabila za Israeli, na maakida wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao; …Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea Bwana; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu. 1 Nyakati 29: 5,6,9

Je wewe leo unamtolea Mungu kwa hiari? Unaweza kutoa kwa namna nyingi, sadaka yako au zaka yako kanisani, lakini pia msaada wako kwa wahitaji, kama yatima, wafungwa, jirani aliye na njaa au shida fulani, yote haya yanafanya watu wengine kufurahi kwa ukarimu wako na Mungu anakupa Baraka kwa majitoleo yako. Je, upo tayari kujitoa kwa moyo ili ujiweke wakfu leo kwa Bwana?

Mungu akubariki sana.

Toa Haki

Mpendwa,

Haki ni kitu muhimu katika maisha yetu ya kila siku, je wewe ni mtu wa haki; haki kwa unayekutana naye barabarani, kama wewe una madaraka, unaotahaki kwa walio chini yako, wewe mwanafamilia, unatoa haki sawa kwa wanafamilia?, na kama una msaidizi wa nyumbani, je unampa haki yake ipasavyo? Mungu anapenda tuwe watu wa kutoa haki, na unapokuwa mtu wa haki, Baraka nyingi unapata, kama neno linavyotuambia “Bali wenye haki wataishi milele na thawabu yao i katika Bwana, na kutukuzwa kwao kumekuwa kweke Yeye aliye juu.” Hekima ya Suleimani 5:15-16.

Basi mpendwa mwombe Bwana Mungu akupe moyo wa kuwa mtu wa haki daima.

Amina

Tafuta kwa na Amani na watu wote

Mpendwa,

Ili kuweza kumwona Mungu  ni lazima kuwa mtakatifu, kuwa mtu safi katika roho yako. Kuwa mtakatifu kunaanza na kuwa na Amani an watu wengine. Mpendwa , tunatakiwa kuomba neema ya Mungu ili tusiwe na uchungu ndani ya mioyo yetu, na hasa uchungu wa kushindwa kusamehe. Kwa kuwa na furaha na amani tutaweza kushiriki uzima wa melele, neno linatuambia “ tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;  mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.  Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi. Waenbrania 12:14-17. Basi wakati ni sasa wa kutafuta Amani, kwani usije ukajikuta utafatuta nafasi ya kutubu na usiipate.

Mungu wa milele nipe Amani na watu wote. Amina

Baraka za Mungu ziwe juu yako.

Wasaidizi

Mpendwa,

Sio kila kitu unaweza kukifanya peke yako, mitume waliona kuwa ni vema kuwa na wasaidizi kwa ajili ya shughuli za mezani wakati wao wakilitangaza neno la Mungu, kama neno linavyosema “Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.  Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;  ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.

Nawe vivyo hivyo katika maisha ya kila siku , kuna mambo ambayo ni lazima kuyafanya wewe mwenyewe na kuna mengine unaweza weka wasaidizi, kwa namna hii unajipa nafasi kwa mambo hayo.

Mungu akubariki.