Salaam za Baraka -Noeli

Mpendwa

Wakati huu tukisheherekea kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, namwomba Mungu , akupe baraka na neema nyingi, uwe na amani na furaha, na Mungu akujalie kila lile analoona linafaa katika maisha.

Wakati huu wa Noeli basi tukuwakumbuke sana wahitaji, kwa kile kidogo Mungu alichotujailia usiache kumshirikisha Jirani na rafiki.

Merry Christmas to you all.

Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.

Malaki 3:1

Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.

Yesu anazaliwa kutokoa katika dhambi.

Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake YESU.

Matayo 1:18-25

Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,  Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia. Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani. Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani. Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli. Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.

Hesabu 3: 5-10

Ole wao wakusudiao mambo maovu

Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi Bwana asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, Sisi tumeangamizwa kabisa; Yeye analibadili fungu la watu wangu; Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu. Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa kamba kwa kura katika mkutano wa Bwana.

Mika 2:1-5

MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote

Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote. Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake.

Isaya 25:7-9

Ukimwacha Mungu, atakukatilia mbali

Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya, basi, Bwana akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni. Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli. Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote. Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya? Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao.

1Wafalme 9:1-9

Simameni imara katika Imani

Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari. Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo. Tena ndugu, nawasihi; (mnawajua watu wa nyumbani mwa Stefana kwamba ni malimbuko ya Akaya, nao wamejitia katika kazi ya kuwahudumu watakatifu); watiini watu kama hawa, na kila mtu afanyaye kazi pamoja nao, na kujitaabisha.Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu.

1 Kor 16:13-17