Baraka

Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu;  Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.

Yuda 1:24-25

Mwaliko wa kumsifu Bwana

Njoni, tumwimbie Bwana, Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, Tumfanyie shangwe kwa zaburi. Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu, Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote. Mkononi mwake zimo bonde za dunia, Hata vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, Na mikono yake iliumba nchi kavu. Njoni, tuabudu, tusujudu, Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!

Zaburi 95:1-7

Mungu anakuletea furaha

Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.  Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu.  Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.  Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.  Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.

Isaya 35:1-6

Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha. Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng’ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake. Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatuWale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope. Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lo lote kwa upendeleo. 
Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi. Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara. Dhambi za watu wengine zi dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.  Vivyo hivyo matendo yaliyo mazuri ya dhahiri; wala yale yasiyo dhahiri hayawezi kusitirika.

1 Timotheo 5:17-24