Wataka nikufanyie nini?

Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

Marko 10:46-52

Kiasi

Mwanangu, jijaribu nafsi yako maadamu u mzima, uviangalie vitu visivyokufaa, usijipatie hivyo. Kwa maana si vitu vyote viwafaavyo watu wote, wala siyo kila mtu apendezwaye na kila kitu. Usione uchu wa anasa yoyote, wala usiwe na choyo kwa habari ya vyakula vyako. Yaani, katika wingi wa vyakula kuna ugonjwa, na ulafi uzidio waleta msokoto wa tumbo. Wengi wamekufa kwa sababu ya kula kwa pupa, bali mwenye kujihadhari atauzidisha uzima wake.

Yoshua bin sira 37:27-31

Mtumaini BWANA

Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu. Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.

Mithali 3:3-6