Tafuta faida ya wengine pia

Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo. Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake. Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri;maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.

1 Wakorinto 10:23-26

Kuwa mtu Uthabiti na wa kujiweza katika ufanyalo

Usipepete kwa kila upepo, Wala usiipitie kila njia.Uwe mtu thabiti wa akili, Na liwe moja neno lako. Uwe mwepesi wa kusikia, Na mzito wa kutoa jibu. Ikiwa unayo akili, umjibu jirani yako; La! Huna, tia mkono wako kinywani pako. Heshima na aibu zina usemi, Na ulimi humwangamiza mtu.Usiitwe msingiziaji, Wala usisengenye kwa ulimi. Juu ya mwizi inakaa aibu, Na hukumu humsibu mnafiki. Usiwe fisadi katika jambo kubwa wala dogo; Wala usipate kuwa adui badala ya rafiki.

Yoshua bin sira 5:9-15

Wana amani nyingi aipendao sheria yako,

Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako. Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele. Wakuu wameniudhi bure, Ila moyo wangu unayahofia maneno yako. Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza. Ee Bwana, nimeungojea wokovu wako, Na maagizo yako nimeyatenda. Nimeyashika mausia yako na shuhuda zako, Maana njia zangu zote zi mbele zako.

Zaburi 119:157, 160-161, 165-166, 168

Rafiki wa Dunia, ni adui wa Mungu

Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!  Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.

Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.

Yakobo 4:1-10

Usisitesite kumfuata Yesu

Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

Matayo 8:18-22

Bwana Atakupigania na Utafurahi

Jipe moyo, Ee Yerusalemu! Yeye aliyekuita kwa jina lako atakufariji. Ole wao waliokutesa Na kuyafurahia maangamizo yako! Ole wa mji uliowatumikisha watoto wako! Ole wake yeye aliyewachukua wana wako! Maana kama  alivyokusimanga katika maanguko yako Na kuufurahia uharibifu wako,Ndivyo atakavyouhuzunikia ukiwa wake mwenyewe. Nitaondoa majisifu yake juu ya wingi wa watu wake, Na majivuno yake yatageuka kuwa kilio, Kwa kuwa moto utamshukia kutoka kwake Aliye wa Milele, Nao utadumu sana. Naye atakaliwa na majini muda wa siku nyingi. Ee Yerusalemu, tazama upande wa mashariki, Uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu. Angalia! Wana wako wanakuja uliowaaga, Wanajikusanya toka mashariki hata magharibi Kwa neno lake Yeye Aliye Mtakatifu, Wakiufurahia utukufu wa Mungu.

Baruku 4:30-37

 

Neema ya Mungu imefunuliwa;

Watumwa na wawatii bwana zao, wakiwapendeza katika mambo yote; wasiwe wenye kujibu, wasiwe waibaji; bali wauonyeshe uaminifu mwema wote, ili wayapambe mafundisho ya Mwokozi wetu Mungu katika mambo yote. Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;  nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.

Tito 2:9-14

neema grace
NEEMA YA MUNGU IMEFUNULIWA

Hekima

Pia nimeona hekima chini ya jua, nayo ni kama hivi, tena kwangu mimi ilionekana kuwa ni neno kubwa. Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga. Basi, kulionekana humo mtu maskini mwenye hekima, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo hapakuwa na mtu ye yote aliyemkumbuka yule mtu maskini. Ndipo niliposema,

Bora hekima kuliko nguvu;

walakini hekima ya maskini hudharauliwa,

wala maneno yake hayasikilizwi. 

Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa,

Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu. 

Hekima ndiyo bora kupita silaha za vita;

Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi.

Mhubiri 9:13-18

courtesy" https://wordforlifesays.files.wordpress.com/2016/10/directory-229117_1920.jpg

 

Salini Hivi – Baba yetu uliye mbinguni

 Basi ninyi salini hivi;

Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,
Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.
Utupe leo riziki yetu.
Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.
Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]
Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Matayo 6:9-15

 

Mpendwa,  kumbuka sala hii ina maombi yote ya muhimu katika maisha yetu, basi daima sali sala hii kwani usalipo unakuwa umeomba yote.

Amina