Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya, basi, Bwana akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni. Bwana akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli. Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote. Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya? Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao.

1Wafalme 9:1-9